Mashabiki wa PSG wabeba mabango yanayoiunga mkono Palestina katikak mechi ya UEFA

Mechi kati ya Paris Saint-Germain na Atletico Madrid katika Ligi ya Soka ya Mabingwa wa Ulaya- UEFA- ilikuwa uwanja wa harakati za kuunga mkono Palestina Jumatano usiku.

Mashabiki waliinua bendera kubwa iliyosomeka: “Palestine Huru” kwa Kiingereza, na ndogo iliyosema, “Mapambano Uwanjani Lakini Amani duniani” kwa Kifaransa kabla ya kuanza kwa mechi hiyo katika uwanja wa Parc des Princes huko Paris. Bango hilo kubwa lilikuwa na picha za Qubbat as-Sakhra katikati ya Msikiti wa Al Aqsa huko al-Quds (Jerusalem) na pia mashabiki walipeperusha bendera za Palestina na Lebanon.

Mashabiki hao wa soka walikuwa wakitaka kukomeshwa kwa vita vya mauaji ya kimbari vya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza na mashambulizi dhidi ya Lebanon. Israel inaendeleza mashambulizi makali dhidi ya Ukanda wa Gaza tangu Oktoba 7, 2023. Mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya takriban watu 43,400, wengi wakiwa ni wanawake na watoto na kufanya eneo la Gaza kutoweza kukalika tena. Israel inakabiliwa na kesi ya mauaji ya halaiki katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki kwa hatua yake katika eneo hilo lililozingirwa.