Vyombo vya habari vya Marekani: Trump anaongoza kwa kura 267 dhidi ya Harris mwenye kura 214

Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, anaongoza katika mbio za kuwania kuingia Ikulu ya White House dhidi ya Makamu wa Rais, Kamala Harris, huku wawili hao wakiendelea kukabana koo katika kura za majimbo muhimu ya Marekani.

Vyombo vya habari vya Marekani vinakadiria kuwa Trump amepata ushindi katika majimbo 25, yakiwemo Texas, Florida na Ohio pamoja na majimbo mengine kadhaa yanayoegemea upande wa Republican.

Wakati huo huo Kamala Harris amepata ushindi katika majimbo 17, yakiwemo majimbo makubwa ya California, New York na Washington.

Hadi tunaingia studio, Trump alikuwa anakaribia kupata ushinda kakmili kwa kuwa na kura 267 mkabala Harris ambaye amepata kura 214 za electoral.

Matokeo yote haya si rasmi hadi maafisa wa uchaguzi wa ndani kote nchini watakapothibitisha matokeo kamili katika siku zijazo.

Mgombea anahitaji kura 270 za uchaguzi ili kupata urais.

Shughuli ya kuhesabu kura za uchaguzi wa urais inaendelea nchini Marekani, baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa jioni ya jana Jumanne kwa saa za Marekani.

Matokeo ya uchaguzi huo yataamua iwapo yatamuweka madarakani Harris na kuwa mwanamke wa kwanza kuliongoza taifa hilo katika historia, au kumrejesha madarakani Donald Trump.