Wanafunzi karibu elfu 12 wa Palestina wameuawa shahidi katika mashambulizi ya Israel Gaza

Wizara ya Elimu ya Palestina imetangaza kuwa, wanafunzi karibu elfu 12 wameuawa shahidi katika mashambulizi ya utawala wa Kizayuni huko Gaza tangu kuanza vita vya mauaji ya kimbari vya Israel dhidi ya eneo hilo Oktoba 7 mwaka jana hadi sasa.

Taarifa ya waizara hiyo imesema wanafunzi karibu elfu ishirini pia wamejeruhiwa katika mashambulizi na mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza; na  wengine 115 wameuawa shahidi katika mashambulizi ya wanajeshi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. 

Kadhalika, tangu kuanza vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza, walimu na wafanyakazi 561 wameuawa shahidi katika eneo hilo na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Jeshi vamizi la Israel limeshambulia pia shule na Vyuo Vikuu 341 na vituo 65 vyenye mfungamano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA). 

Israel na mashambulizi yake ya kikatili dhidi ya shule za Ukanda wa Gaza 

Hivi sasa, zaidi ya asilimia 90 ya shule katika Ukanda wa Gaza zimeharibiwa na kubomolewa kufuatia mashambulizi na mauaji ya kimbari ya Israel, na wanafunzi 639,000 wameshindwa kwenda shule.