Mrithi wa Ten Hag huyu hapa

Manchester, England. Manchester United imemtangaza kocha Ruben Amorim kuwa mrithi wa Eric ten Hag kwenye kikosi hicho baada ya tetesi zilizodumu siku kadhaa.

United iliachana na Ten Hag mwanzoni mwa wiki hii  baada ya kupata matokeo mabaya kwenye Ligi Kuu England na jina pekee lilikuwa linapewa

nafasi kubwa ya kuchukua nafasi yake ni Amorim.

Taarifa iliyotaka muda mchache uliopita inasema kuwa United imempa kocha huyo mkataba wa miaka miwili, lakini atalazimika kubaki kwenye kikosi cha Sporting Lisbon hadi Novemba 11, ndiyo atajiunga na timu hiyo.

“Manchester United inapenda kuwatangazia kuwa Ruben Amorim ndiye kocha mpya wa timu hii kwa sasa.

“Ataungana na timu hii hadi Juni 2027, lakini klabu itakuwa na ruksa ya kumuongezea mwaka mwingine mmoja.

“Amorim atajiunga na timu hii Jumatatu ya Novemba 11 mwaka huu, huyu ni mmoja kati ya makocha bora vijana barani Ulaya kwa sasa, akiwa amefanikiwa kutwaa ubingwa wa Primeira Liga mara mbili nchini Ureno,” imesema taarifa ya United.

Inaelezwa kuwa United wamekubali kulipa ada ya Euro 8.3 milioni ya kuvunja mkataba iliyokuwa inatakiwa na kikosi hicho cha Ureno na tayari kocha huyo amesaini mkataba wa miaka miwili na nusu.

Kocha huyo atakosa michezo mitatu ya United ukiwemo wa wikiendi hii wa Ligi Kuu England dhidi ya Chelsea, Leicester na ule wa Kombe la Europa dhidi ya POK na atajiunga na timu hiyo baada ya mapumziko ya mechi za timu ya Taifa ambapo mechi yake ya kwanza itakuwa dhidi ya Ipswich Town on Novemba 24.

Hata hivyo, pamoja na mshambuliaji wa United wa zamani Ruud va Nisterroy ambaye kwa sasa anashikilia timu hiyo kusema anataka kubaki kwenye kikosi hicho, taarifa ya United haijasema chochote kama atakuwa msaidizi wa kocha huyo raia wa Ureno, bali atasimamia michezo mitatu ijayo.

United kwa sasa inashika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England ikiwa imecheza michezo tisa imeshinda mitatu imetoka sare miwili na kupoteza minne.