Kuendelea vita vya Gaza, kumezidisha malalamiko na hitilafu huko Tel Aviv kadiri kwamba sasa viongozi wa Kizayuni wanatuhumiana wao kwa wao kwa kusema uwongo.
Yair Lapid, kiongozi wa upinzani wa utawala wa Kizayuni, amesema kuhusu idadi halisi ya vifo na majeruhi wa utawala huo katika vita vya Gaza kwamba: “Wanajeshi 11,000 wamejeruhiwa na wengine 890 wameuawa. Wanajeshi 13 pia waliuawa Jumamosi, Oktoba 26, na ikiwa serikali hii haitafanya lolote, wanajeshi 13 zaidi wataongezeka kesho.”
Kiongozi huyo wa upinzani wa utawala wa Kizayuni pia ameongeza kuwa: “Hatuwezi kupuuza ukweli kwamba askari 11,000 wamejeruhiwa na askari 890 wameuawa. Je, tunaweza kusema kwamba kila kitu kinaenda vizuri kama ilivyopangwa?” Lapid pia amesema: “Jeshi halitoi takwimu sahihi. Hizi ndizo takwimu za kweli. Hizi ni takwimu sahihi za waliojeruhiwa na waliouawa. Kila kitu kina mwisho wake; Je, tutaendelea kukubali takwimu bandia hadi lini? Kama mna shaka kuhusu takwimu hizi, tembeleeni hospitali.” Akiendelea kuikosoa serikali ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Lapid, amesema: “Mashambulizi yanaendelea kutokea moja baada ya jingine katika kipindi cha Itmar Ben Gvir, ambaye ni waziri wa kushindwa kitaifa.”
Matamshi ya Lapid yanatolewa katika hali ambayo familia kadhaa za mateka wa utawala wa Kizayuni zilivuruga hafla ya hotuba ya Waziri Mkuu wa utawala huo kuhusiana na operesheni ya “Kimbunga cha al-Aqsa” na kumshambulia kwa maneno makali.
Pengo na tofauti za kimtazamo kati ya wajumbe wa baraza la mawaziri la Netanyahu zimeongezeka sana katika siku za hivi karibuni, ambapo viongozi wa Kizayuni wamekosolewa vikali kutokana na matukio ya vita vya Gaza na Lebanon. Vyama vya upinzani dhidi ya baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni katika bunge la Knesset vinaendelea na harakati zao za kumuondoa Netanyahu madarakani na kumtuhumu kwa kusema uongo na kutokuwa na uwezo wa kusimamia vita vya Gaza.

Vitendo vya kuzusha mivutano vya Wazayuni wenye misimamo mikali ya kupindukia mpaka katika baraza la mawaziri la Netanyahu akiwemo Waziri wa Usalama wa Ndani Itmar Ben Gvir na Waziri wa Fedha Bezalel Smotrich wanaounga mkono kuendelea vita vya Gaza pia wameshadidisha mgogoro wa ndani huko Tel Aviv. Makamanda wa kijeshi wa utawala wa Kizayuni wameonya kuhusu matokeo ya vita na taathira zake hasi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel), huku Wazayuni wenye misimamo ya kufurutu ada wakitaka kuendelezwa vita vya Gaza na kupanuliwa wigo wa vita huko Lebanon.
Malalamiko ya familia za mateka wa Kizayuni dhidi ya Netanyahu ni mwendelezo wa kushadidi hasira na hitilafu katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni kwa kuahidi kuwatimua Hamas kutoka Gaza, alipanua wigo wa vita katika ukanda huo katika hali ambayo leo hii makundi ya muqawama ya Palestina, Lebanon na eneo yamewapa Wazayuni mapigo makali yasiyoweza kufidika.
Kuendelea vita huko Gaza kumepelekea kufichuliwa hitilafu na mizozo ya ndani katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, ambapo sasa baadhi ya viongozi wa utawala huo wamelazimika kukiri kwamba takwimu zinazotolewa na serikali kuhusu vita hivyo ni za uongo mtupu. Netanyahu kutokuwa na uwezo wa kutatua suala la mateka wa Kizayuni pia kumeongeza malalamiko katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Kutokana na kuongezeka hitilafu baina ya upinzani na baraza la mawaziri na Netanyahu, pamoja na maandamano katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, hali mbaya ya utawala wa Kizayuni itazidi kuharibika zaidi katika siku zijazo.
Wanaharakati wa masuala ya kiraia na waungaji mkono wa wananchi wa Palestina pia wamefanya maandamano makubwa kupinga ukatili na mauaji ya kimbari ya Wazayuni kote Ulaya na Marekani, jambo ambalo limeleta mwamko katika pembe tofauti za dunia kuhusu hali ya kusikitisha ya wananchi wa Palestina. Mshindwa mkuu wa matukio ya eneo hili ni utawala wa Kizayuni ambao unakabiliwa na mgogoro mkubwa wa ndani ambapo katika ngazi za kimataifa pia unatambuliwa kuwa chanzo kikuu cha mauaji ya kimbari huko Ghaza.