
Bwana Elvino Dias, wakili wa mgombea wa uchaguzi wa rais uliopita nchini Msumbiji ameuawa leo asubuhi kwa kupigwa risasi akiwa pamoja na ajenti wa chama kimoja cha siasa nchini humo. Polisi wanasema sababu ya mauaji hayo bado haijajulikana.
Dias alikuwa wakili wa Venancio Modlane, mgomea huru wa kiti cha rais wa Msumbiji, na ameuawa akiwa pamoja na Paulo Guambe, mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa chama cha Podemos, ambacho kinamuunga mkono Mondlane.
Polisi imesema wawili hao wameuawa wakiwa kwenye gari lao katika mtaa wa Malhangalene, moja ya viunga vya mji mkuu Maputo. Waliohusika na mauaji hayo bado hawajulikani.
Tukio hilo huenda likachochea ghasia na machafuko katika nchi hiyo ambayo bado inakabiliwa na hali ya wasiwasi na mivutano kufuatia uchaguzi mkuu wa rais, bunge na magavana. Kwa kawaida Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo ina siku 15 za kutangaza matokeo ya uchaguzi baada ya kufanyika zoezi la uchaguzi.
Mapema Mondlane alizua kizaazaa baada ya kujitangaza kuwa mshindi wa uchaguzi, hatua iliyompelekea kukosolewa vikali na tume hiyo.
Dias alikuwa wakili mashuhuri wa kutetea haki za binadamu nchini Msumbiji naye Guambe akiwa ajenti wa chama cha Podemos katika uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 9.