300 wafanyiwa upasuaji wa macho

Mbeya. Watu 4,000 waliofanyiwa vipimo na madaktari bingwa wa macho wamebainika kuwa na uoni hafifu, kati hao 300 wamefanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.

Katika idadi hiyo watu 3,400 walimepatiwa miwani ya macho bure kulingana na ukubwa wa tatizo, huku watoto wawili wamepewa rufaa ya matibabu zaidi katika Hospitali Rufaa ya Taifa Muhimbili.

Takwimu hizo zimetolewa leo Jumanne Aprili 22, 2025 na mratibu wa kambi ya madaktari bingwa kutoka Taasisi ya The Bilal Muslim Mission Tanzania, Ain Sharif baada ya kuhitimisha kambi ya siku nne iliyohusisha madaktari 68 kutoka hospitali mbalimbali nchini.

Kambi hiyo iliratibiwa na Taasisi ya Tulia Trust kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya kwa lengo la kurejesha tabasabu kwa jamii yenye changamoto ya macho.

Awali, Sharif amesema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, imebainika kuwepo na changamoto kubwa ya tatizo la mtoto wa jicho na trakoma kwa wazee na watoto ambao wanahitaji matibabu maalumu.

“Tumeona ukubwa wa tatizo vipo visababishi mbalimbali, lakini tunamshukuru Mungu kwa idadi hiyo ya watu waliobainika na kupata tiba na kurejesha tabasamu,” amesema.

Sharif amesema walijipanga na timu ya wataalamu kutoa huduma kwa wana-Mbeya ikiwa ni awamu ya pili.

“Gharama za matibabu ya macho ni kubwa lakini Mbunge wenu na Spika wa Bunge, Dk Tulia kwa upendo amejitoa kugharamia matibabu, miwani na dawa sambamba na kusafirisha timu ya madaktari bingwa 68 kuja Mbeya,” amesema.

Dk Tulia ameishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa wa vifaatiba na wataalamu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda, jambo ambalo limerahisisha utoaji huduma ya upasuaji kwa wananchi.

Baadhi ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa macho wakiwa katika Hosptali ya Rufaa Kanda ya Mbeya   kupitia Taasisi ya The  Bilal Muslim Mission Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Tulia Trust. Picha na Hawa Mathias

“Uwekezaji wa vifaatiba na wataalamu umesaidia kurahisisha zoezi la utoaji huduma za upasuaji wagonjwa walio bainika na mtoto wa jicho na hata walipewa rufaa kwenda Muhimbili,” amesema.

Dk Tulia amesema hii ni awamu ya pili kwa Taasisi ya Bilal Muslim Mission Tanzania kwa kushirikiana na Tulia Trust kutoa huduma za uchunguzi wa macho kwa wananchi na kutoa matibabu hususani upasuaji na miwani bure.

“Mwaka juzi jumla ya wananchi 260 walifanyiwa upasuaji lengo ni kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha tunarejesha tabasamu lililopotea kwa jamii wakiwepo wazee,” amesema.

Mzazi wa mtoto Oscar Salehe (5) mwenye kansa ya jicho, Anna Kapindila (40) mkazi wa Mkoa wa Rukwa, amesema kwa miaka mingi amepata changamoto ya namna ya kupata matibabu kwa mwanaye bila mafanikio.

“Nashukuru nimefika Mbeya salama na tayari mwanangu kafanyiwa uchunguzi ambapo tunasafirishwa kwa matibabu zaidi kwenda Hosptali ya Taifa Muhimbili kupitia Taasisi ya Bilal Muslim Mission Tanzania,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *