Nigeria. Baada ya mwanamuziki kutoka Nigeria Innocent Idibia ‘2Face’ kutangaza kuachana na mkewe Annie Idibia, baada ya kudumu naye kwenye ndoa kwa miaka 13. Hatimaye jana Februari 12,2025 amemvisha pete Mbunge wa Jimbo la Edo, Natasha Osawaru.

Kufuatia video mbalimbali zinazoendelea kusambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonesha msanii huyo akimvisha pete mbunge huyo.
Utakumbuka Februari 11, 2025 2face kupitia ukurasa wake wa Instagram alichapisha picha ya mbunge huyo akiambatanisha na ujumbe wa kudai kuwa ndio mwanamke atakayefunga naye ndoa tena.

“Natasha ni mwanamke mchanga, mwelevu, na wa ajabu. Nampenda, anapendeza, na nataka kumuoa,” amesema 2Face huku akisisitiza kuwa Mbunge huyo asihusishwe na talaka yake na badala yake lawama zote ziende kwake.

Msanii huyo aliyewahi kutamba na ngoma ya ‘African Queen’. Mwishoni mwa Januari 2025 alitangaza kutengana na aliyekuwa mke wake baada ya kudumu naye kwa miaka 13 huku akidai kuwa kwa sasa wapo katika taratibu za kupeana talaka.

2face akiwa na aliyekuwa mkewe Annie
Aidha kutokana na watu kuwa na maoni tofauti mwanamuziki huyo aliamua kufuta chapisho hilo huku akiwaacha mashabiki na wadau wake njia panda kama ni kweli alichokizungumza au ni kiki.