Dar es Salaam. Wengi wanaposikia wimbo ‘Mama Neema’ wa kwake 20 Percent, wanakumbuka miaka 13 iliyopita. Kwani wimbo huo ulichukua usikivu wa hali ya juu katika kipindi hicho.
Akizungumza na Mwananchi 20 Percent amesema alipoanza muziki haikuwa ngumu kukubalika kwenye jamii.
“Siku zote asili yangu ya muziki ipo kwenye damu na ninashukuru wakati naanza muziki haikuwa ngumu. Kutokana na uhalisia wa ujumbe wangu na kusema kweli mimi huwa siongopi katika muziki ndiyo maana niliutambulisha vizuri,” amesema

Hawezi kujishusha kwa sababu ya pesa
Msanii huyo amesema licha ya kushuka kimuziki kwa sasa, hawezi kujishusha kwa mtu hasa aliyemzidi pesa.
“Ifike mahali kila mtu ajiamini, kama mimi siwezi kutoka nikaenda kwa mtu kumnyenyekea kwa sababu yuko juu na ana kipato.
“Ukiona binadamu anaacha kujiamini huo unakuwa utumwa. Kuna mtu mmoja aliwahi kuwa chini ya wadogo zake lakini ameishia kudharirika tu na wadogo zake wakanufaika kupitia yeye. Nataka wasanii wengine watambue kwamba mtu akitaka kukusaidia lazima na yeye afaidike,” amesema Twenty.

Sababu ya kutosikika kama mwanzo
Msanii huyo amesema muziki ni kama chakula una wakati wake, ndiyo maana kwa sasa hasikiki kama zamani.
“Ukitaka kula huwezi ukala kila siku chakula cha aina moja. Sasa inategemea kwa sasa watu wanapenda muziki wa aina gani na ndiyo maana kwa wakati huu muziki wa aina yangu hausikilizwi sana kama zamani.
“Lakini siyo kwamba sifanyi muziki la hasha nafanya ila ni ngumu kwa sasa muziki wa aina yangu kusikika masikioni mwa watu kwa sababu sasa tuna vizazi tofauti kama vizazi vya Instagram haviwezi kupata muziki wangu kwa urahisi,” amesema Twenty
Hata hivyo ameongezea kuwa siku hizi wasanii wamejikita sana kwenye muziki wa kuiga na siyo Bongo Fleva yenyewe.
“ Sasa hivi wanamuziki wamekuwa wakiiga sana muziki wa nje yaani hawashughulishi akili zao. Hii itaendelea kwa Tanzania kutokana na wasanii wengi badala ya kufanya kazi ya kutoa ujumbe, wao wanafanya biashara,” amesema