
Dar es Salaam. Wafanyabiashara 142 wa soko Kuu la Kariakoo waliokatwa mara ya pili katika orodha ya wanaotakiwa kurudi sokoni hapo, wameelezwa kuwa hawana vigezo, hivyo kutakiwa kuomba upya.
Akizungumza leo Jumatano Aprili 9,2025 na Mwananchi Digital, Ofisa Uhusiano Mkuu wa Shirika la Masoko Kariakoo, Revocutus Kasimba amesema baada ya kupitia barua zao walizoandika kuomba warejeshwe, imebainika ni kweli hawakuwa na vigezo vya kurudishwa na hivyo orodha ya mwisho ilikuwa sahihi.
Katika orodha hiyo iliyowekwa hadharani Januari 31,2025, baada ya kufanyika uhakiki wa pili ilionyesha wafanyabiashara 1,520 kati ya 1,662 waliokuwepo kabla ya soko kuungua, ndio wanaopaswa kurejeshwa sokoni hapo.
Hii ikiwa ni tofauti na orodha ya kwanza iliyoonyesha waliotakiwa kurudi walikuwa ni 819, orodha iliyogomewa na wafanyabiashara hao.
Hata hivyo, ili kufikisha kilio chao hicho Julai 12, 2024 walikusanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja kisha kuandamana hadi ofisi ndogo za Chama cha Mapinduzi, Lumumba jijini hapa.
Julai 13,2024 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alikutana nao na kuridhika na hoja zao, ambapo pamoja na mambo mengine aliamuru majina 819 yaliyokuwa yamepitishwa yaondolewe kwenye mfumo na kufanyika uhakiki upya kwa kuwashirikisha kwa karibu viongozi wao.
Soko la Kariakoo liliungua Julai 10, 2021, ambapo Serikali ilitoa Sh29 bilioni ili lifanyiwe ukarabati ambao ulikwenda sanjari na ujenzi mpya wa soko dogo.
Nyakati zote ujenzi ukiendelea , wafanyabiashara hao walihamishiwa katika masoko ya Karume, Machinga Complex na Kisutu kuendelea na shughuli zao.
Vigezo vilivyotumika kuwarejesha
Akieleza vigezo vilivyotumika kuwarejesha wafanyabiashara hao, Kasimba amesema ni pamoja na kutokuwa na deni na ambaye alikuwa na mkataba wa upangishaji na Shirika.
Katika hili amesema baada ya soko kuungua na nyaraka zilizokuwepo ndani za mikataba, waliwaita kwa mara nyingine kuandikishiana upya mikataba.
Kigezo kingine amesema ni aliyekutwa eneo hilo la soko wakati moto umetokea na katika nyaraka zake ilionyesha alikuwa analipa kodi ya eneo hilo kwa muda mrefu kwa kutumia jina lake.
“Tulichobaini hapa na kamati ni kwamba kuna watu walikuwa wamepangisha maeneo haya kwa wengine na wao kwenda kujishughulisha na kazi zingine, walikuwa walipaji wazuri na walilipa kwa kutumia majina yao, wamiliki tuliwanyang’anya maeneo hayo na kuwapa wao,” amesema Kasimba.
Aidha waliokuwa wasaidizi wa wafanyabiashara nao wamepata maeneo baada ya kamati kuwachukulia kwamba ni wafanyabiashara ambao nao sasa wamekuwa, hivyo wapewe maeneo ambapo wasaidizi 123 wamebahatika katika ofa hiyo.
Aidha kwa wale waliokuwa wanamiliki eneo zaidi ya moja, nao waliachiwa moja.
“Tulibaini kuwa miongoni mwa viongozi wa wafanyabiashara kuna watu wanamiliki maeneo zaidi ya sita, hawa tumewabakishia moja tu mengine wamepewa wengine wenye sifa.
Vilevile kwa waliochiwa maeneo kama warithi na baadaye kugombana wenyewe kwa wenyewe kwa kutoelewana nani awe msimamizi, nao wamewanyang’anya ili kuepusha migogoro hapo baadaye.
Walichosema wafanyabiashara
Wakati Shirika la Masoko likitoa msimamo huo, baadhi ya wafanyabiashara wamesema watadai haki yao hadi dakika za mwisho, ambapo wameeleza kuwa wameshaanza kuwasilisha barua za malalamiko kwa uongozi wa juu.
Mwenyekiti Soko la Wazi, Hussein Shomari amesema hawaelewi kwa nini kamati iliwaweka wenzao wengine kando katika orodha, ukizingatia uhakiki huo waliufanya kwa kushirikiana.
Hata hivyo Shomari amesema kilichowasikitisha zaidi ni kuwa licha ya makubaliano kwamba kabla ya orodha kutoka waipitie kwanza, lakini hawakufanya hivyo na ndio maana changamoto hizo zimejitokeza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa soko dogo, Msuya Minja amesema kwake wafanyabiashara 40 kati ya 225 waliokuwepo kabla ya soko kuungua wamekatwa katika orodha hiyo.
“Hili limetusikitisha ukizingatia watu tunajuana tuliokuwa tunafanya biashara pale, sasa kama orodha zote mbili zimewakataa, tunaziachia mamlaka ziamue kwa kuwa sasa tukiongea tena tutaonekana ving’ang’anizi na tunaamini meneja aliyeteuliwa hivi karibuni na Rais Samia Suluhu Hassan atalifanyia kazi hili kwa umakini,” amesema Minja.
Mwenyekiti wa Vigoli (maduka kwenye kuta za soko), Abdul Karim amesema wao wanashukuru wote wamepata na kueleza wanachosubiri sasa ni kuambiwa lini soko linafunguliwa.
Danadana za kulifungua zaendelea
Katika hatua nyingine, danadana za kulifungua soko hilo zimeendelea, ambapo kila wakati kumekuwa na tarehe tofauti za kuanza kwake kazi zinazotolewa na uongozi wa Shirika.
Soko hilo kwa mujibu wa Mwenyekiti wa bodi ya Shirika, Hawa Ghasia, sasa litafunguliwa rasmi mwezi huu (Aprili), 2025.
Hawa aliyasema hayo katika hafla ya kumkabidhi ofisi Meneja mpya wa shirika hilo, Ashraph Yusuph Abdulkarim iliyofanyika Aprili 4,2025 katika ofisi za shirika hilo, zilizopo Kivukoni jijini Dar es Salaam.
Kauli hiyo inatofautiana na ile aliyowahi kuisema Januari 29, 2025, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu urejeshwaji wa wafanyabiashara sokoni hapo baada ya kuketiwa kwa kikao cha bodi Januari 27,2025.